Msanii Zuchu hatimaye amevunja kimya chake ikiwa ni siku chache tu baada ya walimu wakuu wawili kushushwa vyeo vyao kufuatia klipu ya wanafunzi katika shule zao wakicheza densi ya wimbo wa Honey.
Mkoani Songwe, walimu wakuu wawili wa shule za msingi walipoteza vyeo vyao na kufanywa kuwa walimu wa kawaida tu kufuatia klipu hizo zilizosambaa watoto shuleni wakicheza densi ya wimbo huo.
Taarifa za awali zilidai kwamba waziri wa elimu katika taifa hilo alitoa amri ya wawili hao kushushwa vyeo mara moja kutokana na kukubali watoto kuchezewa nyimbo alizozitaja kuwa hazina maadili shuleni.
Baada ya habari hizo kusagaa kote mitandaoni, msanii Zuchu katika kipindi cha Jana na Leo kwenye Wasafi FM, alisema kwamba binafsi aliumia pakubwa kutokana na agizo hilo la wizara ya elimu kuwashusha vyeo walimu.
“Binafsi nimeumia kwa sababu walimu hao walikuwa wanapata mshahara mzuri lakini baada ya kushushwa cheo pengine hata maslahi yao yatapungua,” alisema kwa mahojiano ya njia ya simu na mtangazaji Baba Levo.
Msanii huyo pia alisisitiza kwamba yeye haoni shida yoyote kwa watoto kula burudani kwa kutumia wimbo wake.
“Mimi sioni shida kwa sababu katika wimbo wangu mashairi yako sawa na sioni tatizo kwa watoto kuucheza wimbo wangu,” aliongeza.
Watoto hao walikuwa wanacheza wimbo huo baada tu ya kampuni moja kupeleka msaada katika eneo hilo na hili lilitokea baada ya kukamilika kwa hafla rasmi na kupisha kipindi cha burudani.