Rais wa Marekani Joe Biden anasema ataangalia uwezekano wa vikwazo binafsi dhidi ya Vladimir Putin iwapo Urusi itaivamia Ukraine.
Bw Biden alisema kunaweza kuwa na "madhara makubwa" kwa dunia iwapo Urusi itachukua hatua kwa taifa , lililoko katika mpaka wa kusini -magharibi.
Kauli zake zimekuja huku viongozi wa Magharibi wakirudia tahadhari zao kwamba Urusi italipa gharama nzito kwa uvamizi.
Urusi imeishutumu Marekani na wengine kwa "kuzidisha wasi wasi " juu ya suala na inakanusha kuwa inapanga kuingia Ukraine.
Hatahivyo, utawala wa Moscow umeongeza wanajeshi wake kwenye mpaka na Ukraine , huku wanajeshi wapatao 100,000 wa Urusi wakipelekwa katika eneo hilo la mpaka.
Akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Bw Biden alijibu "ndio" wakati alipoulizwa iwapo anafikiria binafsi kuwa anaweza kumuwekea vikwazo rais wa Urusi binafsi iwapo kutakuwa na uvamizi dhidi ya Ukraine.
Alisema kuwa hatua ya aina hiyo ya kuvuka mpaka wa Ukraine itakuwa na " madhara makubwa katika dunia nzima" na inaweza kusababisha "uvamizi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu vita kuu vya pili vya dunia".
Bw Biden aliongeza kuwa atalazimika kuongeza uwepo wa Nato mashariki mwa Ulaya.
"Lazima tuliweke wazi kwamba hakuna sababu yeyote kwa mjumbe yoyote wa Nato kuwa na wasiwasi…Nato inaweza kujilinda ," alisema.
Lakini alirudia kuwa hakuna mipango ya kutuma vikosi vya Marekani ndani ya Ukraine kwenyewe.
Urusi ilijibu kwa kauli za hasira na kuishutumu Marekani na NATO kwa "kuijaza" Ukraine kwa silaha na washauri wa magharibi.
"Hakuna maelezo ya kile ndege za kijeshi za Marekani zinachokifanya karibu na mwambao wa Ukraine," alisema mjumbe wa kudumu wa Moscow katika Umoja wa Mtaifa katika taarifa yake.
Kwa sasa Urusi hutoa takriban theluthi moja ya mafuta ghafi na gesi inayoingizwa katika Muungano wa Ulaya.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kuwa washirika wa Magharibi watajibu uvamizi wowote kwa vikazo''vikali''vya kiuchumi, akiongeza kuwa Uingereza inajiandaa kupeleka vikosi vyake ili kuwalinda washirika wa NATO katika kanda.
Alizungumzia suala la kuwekea marufuku Urusi kuanzia mfumo wa wepesi wa malipo ya kimataifa, hatua ambayo maafisa wa ngazi ya juu wa Urusi walisema ina maanisha Ulaya haitaweza kulipa na kupokea malipo ya bidhaa zinazotoka Urusi.
Wakati huo huo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa mazungumzo na Moscow yataendelea.
Atazungumza kwa njia ya simu na Bw Putin Ijumaa, aliongeza, na kutaka ufafanuzi kuhusu nia za Urusi kwa Ukraine.
Wakati wa mazungumzo ya mzozo Jumatatu, mataifa yenye nguvu ya magharibi yalikubaliana kuweka vikwazo "visivyo vya kawaida'' dhidi ya uvamizi wa Urusi iwapo itavamia.
Marekani wameweka pia wanajeshi 8,500 katika hali ya tahadhari -kwa sehemu moja kwa ajili ya kuimarisha vikozi vya washirika wake wa Nato-ambao Urusi inasema wamesababisha "hofu kubwa".
Washington pia imemuonya mshirika wa Urusi Belarus kwamba "ikakabiliana na jibu la haraka lililoamriwa" iwapo itasaidia katika uvamizi.
Utawala wa Kremlin umesema kuwa unaiona Nato kama tishio la usalama, na inadai kuwepo kwa hakikisho la kisheria kwamba muungano huo hautapanuka mashariki zaidi, ikiwa ni pamoja na katika jirani wake Ukraine. Lakini Marekani imesema kuwa tatizo ni uchokozi wa Urusi, na sio kupanuka kwa Nato.
Hofu ya uvamizi imezifanya balozi za Magharibi mjini Kyiv kuwaondoa wafanyakazi wake.
Lakini Rais wa ukraine Volodymyr Zelensky alijaribu kulihakikishia taifa lake usalama katika hotuba yake ya kitaifa kwenye televisheni Jumanne.
"Hakuna sherehe, hakuna ndoto za kitoto, kila kitu sio rahisi…Lakini kuna matumaini ,"alisema. "Linda mwili wako dhidi ya virusi, ubongo wako dhidi ya uongo, moyo wako dhidi ya wasi wasi."
Alisema kuwa anafanya juhudi za kupanga mkutano na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Urusi.
Urusi ilichukua eneo la Ukraine kabla, wakati ilipotenga Crimea mwaka 2014. Baada ya vikosi vya Urusi kunyakua udhibiti , Crimea ilipiga kura kujiunga na Urusi katika kura ya maoni ambayo mataifa ya Magharibi yaliona kama haramu kisheria.
Waasi wanaoungwa mkono na Urusi pia wanadhibiti maeneo ya mashariki mwa Ukraine karibu na mipaka ya Urusi. Mzozo huo umegarimu maisha ya watu wapatao 14,000, huku mkataba wa mwaka 2015 ukiwa bado haujatimizwa.