Klabu ya Manchester United imeiambia Inter Milan kwamba iko tayari kutoa Pauni Milioni 40 ili kufanikisha usajili wa Mlinda Lango wao, Andre Onana, kwa mujibu wa ESPN.
Mazungumzo na wawakilishi wa Onana yaliyoanza juma lililopita, yamekuwa na tija, na United iko tayari kutoa kiasi kinachotakiwa na Inter pamoja na nyongeza.
Vyanzo viliiambia ESPN kwamba hesabu ya Inter ni zaidi ya Pauni Milioni 50, lakini kuna matumaini kwamba maelewano yanaweza kufikiwa.
Timu hiyo ya Serie A inafahamu nia ya Onana kuhamia Old Trafford, ambako ataungana tena na kocha wake wa zamani kule Ajax, Erik ten Hag.
Ten Hag amemtambua mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon kama shabaha yake anayopendelea zaidi inapotafuta kipa mpya msimu huu wa joto.
Vyanzo viliiambia ESPN kwamba United bado inaendelea na mazungumzo ya ana kwa ana na David de Gea kuhusu hali ya mkataba wake. Mkataba wa De Gea uliisha Juni 30 na sasa ni mchezaji huru.
Dean Henderson amekuwa akifanya mazoezi pale Carrington juma jhili baada ya kumalizika kwa muda wake wa mkopo kule Nottingham Forest.
Vyanzo viliiambia ESPN kwamba Forest inataka kumsaijili Henderson kwa mkataba wa kudumu na, kwa jinsi mambo yanavyoendelea, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ana uwezekano mkubwa wa kuwa sehemu ya kikosi cha United kwa ajili ya ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani, itakayoanza New York Julai 20.