Xavi akataa kuicheka Real Madrid

Meneja wa Mabingwa wa Soka nchini Hispania FC Barcelona, Xavi Hernandez amekataa kuiponda Real Madrid baada ya kuondoshwa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kwa kufungwa mabao 4-0 na Manchester City katika Uwanja wa Etihad, juma lililopita.

Kutokana na ushindi huo, Manchester City itakutana na Inter Milan kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa Jiji la Istanbul Juni mwaka huu.

Xavi amekiri kuwa mashabiki wa FC Barcelona watakuwa wamefurahia wapinzani wao ambao wameshinda taji hilo mara tano katika kipindi cha miaka 10, lakini kwa upande wake alichagua kuzungumzia upande wa ubora wa Manchester City kwenye mchezo huo.

“Sipendi kutumia neno kipigo katika soka,” amesema Xavi kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu mchezo huo.

“Maneno kama hayo na kufeli hayajengi. Tazama, City walikuwa bora sana kwenye mechi ile na walitumia faida ya ubora wao vizuri.

“Haikuwa hivyo katika Uwanja wa Santiago Bernabeu kwenye mchezo wa kwanza, lakini kwa ujumla walistahili kushinda. Kwa sasa wao ni timu bora duniani,”


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii