Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad A.C Juan Carlos Garrido Fernández ameichimba mkwara Simba SC kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC ipo mbele kwa bao 1-0, baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, juzi Jumamosi (April 22), bao likifungwa na Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke.
Kocha Fernandez amesema wamekubali kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Simba SC, na sasa wanachokifanya ni kuhakikisha wanashinda mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa mjini Casablanca-Morocco mwishoni mwa juma hili.
Wydad A.C itaikaribisha Simba SC katika Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca, Jumamosi (Aprili 28) ikitakiwa kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri au zaidi, ili isonge mbele katika hatua ya Nusu Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.