Erling Haaland Awakosha Man City Kwa Huduma yake, Wamwandalia Mtakaba Mwingine Mnono

Klabu Bingwa nchini England Manchester City inajiandaa kumpa mkataba mpya Mshambuliaji Erling Haaland baada ya kuwakosha kwa huduma yake moto katika msimu huu wa kwanza kwenye Ligi Kuu England, imeelezwa.

Man City ilinasa saini ya Haaland kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya Pauni 51.2 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Baada ya kuonyesha kiwango bora huko Etihad Pep Guardiola anafikiria kumpa dili jipya, Mkataba wake wa awali ulikuwa na kipengele cha kuvunjika kwa Pauni 150 milioni itakapofika mwakani, lakini hicho kipengele kilifutika baada ya kocha Guardiola kusaini mkataba mpya, Novemba mwaka jana.

Bado haifahamiki kama kwenye dili jipya la Haaland kutakuwa na kipengele cha aina hiyo, lakini Man City wanataka kumpa mkataba mpya ili kuwakata ngebe Real Madrid wanaosumbuka kuhitaji huduma ya straika huyo wa kimataifa wa Norway.

Haaland, 22, ameanza maisha Man City kwa moto kwelikweli, ambapo katika mechi 40 alizocheza amefunga mabao 47.Usiku wa jana Jumatano alikuwa uwanjani Allianz Arena kuitumikia timu yake katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Bayern Munich, huku ile ya kwanza Man City ilishinda 3-0, na straika huyo akiwa miongoni mwa waliotikisa nyavu katika mchezo huo uliofanyika uwanjani Etihad.

Atakayepenya katika mchezo huo atakutana na Real Madrid nusu fainali baada ya miamba hiyo ya Hispania kuitupa nje Chelsea kwa mabao 4-0 katika hatua ya Robo Fainali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii