Fei Toto Aahidi Ushindi Stars Dhidi ya Uganda Kufuzu AFCON

KIUNGO wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Feisal Salum ‘Fei Toto’ baada ya kutua nchini Misri, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu maandalizi ya mechi yao dhidi ya Uganda kufuzu AFCON.

Fei Toto amesema wamejiandaa vizuri na wanaahidi ushindi kwa Watanzania, huku akiweka wazi kuwa, siku zote haijawahi kuwa rahisi kucheza dhidi ya Uganda.

Kiungo huyo alitua kambini hivi karibuni kuungana na wenzake kwenye mji wa Ismailia ambako utachezwa mchezo huo kesho Ijumaa.“Kweli kuna wachezaji wapya na mwalimu mpya, Uganda tunawaheshimu, ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri, ila tutaipambania Taifa Stars ili tupate matokeo.

“Najua siyo jambo rahisi, lakini ni muhimu zaidi kwa timu yetu kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu. Katika mechi mbili Watanzania watuombee dua na tutapata matokeo mazuri kwa uwezo wake Mungu,” alisema.

Taifa Stars itacheza mechi mbili dhidi ya Uganda katika kuwania kufuzu michuano ya AFCON itakayofanyika mwaka 2024 nchini Ivory Coast.

Kesho Ijumaa ikianzia ugenini nchini Misri dhidi ya Uganda, kisha Machi 28, timu hizo zitarudiana jijini Dar. Kwenye Kundi F, Taifa Stars ipo na timu za Algeria inayoongoza kundi hilo, Niger na Uganda.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii