Mwanasoka Wa Zamani Wa Man-United, John O’Shea Ateuliwa Kuwa Kocha Msaidizi Wa Jamhuri Ya Ireland

BEKI wa zamani wa Manchester United, John O’Shea, ameteuliwa kuwa kocha msaidizi katika timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland ambayo sasa inanolewa na mkufunzi Stephen Kenny.

O’Shea, 41, anakuwa kocha msaidizi baada ya kudhibiti mikoba ya kikosi cha chipukizi wa U-21 nchini Ireland kwa takriban miaka mitatu iliyopita.

O’Shea ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa kikosi cha Stoke City, alihitimu ukufunzi wa kiwango cha Pro Licence mnamo Disemba 2022. Anatarajiwa kujumuisha majukumu yake mapya yatakayoanza kwa mechi za kufuzu kwa fainali za Euro 2024 na kusimamia pia kikosi cha Stoke City.

Difenda huyo aliwahi kuchezea Ireland mara 118 na ndiye wa tatu katika orodha ya wanasoka wanaojivunia kuwajibikia kikosi hicho mara nyingi zaidi.

“Ni fahari tele kuwa sehemu ya benchi ya kiufundi ya timu ya taifa ya Ireland,” akasema O’Shea aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichonogesha fainali za Euro 2012 na 2016.

Akivalia jezi za Man-United, sogora huyo aliwahi kunyanyua mataji matano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Jamhuri ya Ireland wamepangiwa kuanza mechi za kufuzu kwa fainali za Euro 2024 kwa mechi ya nyumbani dhidi ya Ufaransa mnamo Machi 27, 2023, siku tano baada ya kuwa wenyeji wa Latvia katika pambano la kirafiki jijini Dublin.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii