Young Africans yamlima barua Feisal Salum

Kwa mara nyingine tena Uongozi wa Young Africans umemwandikia Barua Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ ya kumtaka kurejea kambini kujiunga na wachezaji wenzake.
Young Africans imefanya hivyo, baada ya kukiri kupokea maamuzi ya marejeo ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu suala la kiungo huyo.

Taarifa ya Young Africans imeeleza kuwa, baada ya kupokea maamuzi hayo, Uongozi wa Klabu hiyo umemwandikia Barua Feisal Salum kumtaka aripoti kambini haraka iwezekanavyo na kuendelea kuutumikia mkataba wake kama mchezaji wao halali mpaka tarehe 30, Mei 2024, kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.

Hata hivyo taarifa hiyo imesisitiza Klabu ya Young Africans iko tayari kumpokea Feisal Salum na kumjumuisha kwenye kikosi, na kwa kuzingatia sera na utaratibu wa Klabu hiyo katika kuwaongezea mikataba wachezaji wake wanaofanya vizuri.

“Uongozi wa Yanga uko tayari kuendelea na mazungumzo na Feisal Salum Abdallah na wawakilishi wake juu ya kuboresha mkataba wake, kama wataridhia.” imeeleza taarifa hiyo.





Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii