Jumuia ya kimataifa yaingilia mzozo wa kisiasa wa Somalia

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Ari Gaitanis amesema Jumatano kwamba  Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa mengine wanafanya mazungumzo na waziri mkuu wa Somalia  pamoja na rais wakati wakiwarai kupunguza taharuki ya kisiasa inayohofiwa kupelekea ghasia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, maafisa hao wameongeza kusema kwamba waziri mkuu Mohammed Hussein Roble alifanya mazungumzo na afisa wa ngazi ya juu wa Marekani kuhusu mzozo wa kisiasa nchini mwake, likiwa suala ambalo wachambuzi wanasema linahujumu juhudi za serikali za kukabiliana na makundi ya kigaidi kama vile al Qaeda na al Shabaab. 

Mazungumzo ya Jumatano yanasemekana kuhusisha Marekani, Uingereza na EU miongoni mwa wengine. Baadhi ya watu waliokutana nao ni rais Mohamed Abdullahi Mohamed pamoja na kundi la wagombea wanaolenga kushindana naye kwenye uchaguzi wa rais. Gaitanis ameongeza kusema kwamba lengo la mazungumzo hayo ni kuwasihi viongozi hao kuweka maslahi yao kando na badala yake wazingatie mapungufu yalioko kwenye mchakato wa uchaguzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii