Claudio Ranieri Arejea Italia Kuwa Kocha Wa Klabu Ya Cagliari Aliyowahi Kuinoa Zaidi Ya Miaka 30 Iliyopita

CLAUDIO Ranieri ameaajiriwa tena kuwa kocha wa Cagliari, zaidi ya miaka 30 tangu apokezwe mikoba ya kudhibiti kikosi hicho cha soka ya Italia kwa mara ya kwanza.

Umaarufu katika ulingo wa ukufunzi ulianza kumwandama akiwa kocha wa Cagliari kati ya 1988 na 1991 ambapo alifaulu kuongoza klabu hiyo kupanda ngazi kutoka Serie C hadi Serie A.

Ranieri, 71, ametia saini mkataba wa kunoa Cagliari hadi 2025, hiyo ikiwa ni kazi yake ya kwanza tangu atimuliwe na Watford mnamo Januari 2022.

“Narejea Cagliari – kikosi ambacho nimekijua kwa muda mrefu. Hata nilipoagana nacho 1991, niliahidi wadau wa klabu hiyo kwamba ningerudi baadaye kuwa sehemu ya shughuli,” akasema mkufunzi huyo raia wa Italia.

Ranieri anajaza pengo la kocha Fabio Liverani aliyepigwa kalamu na Cagliari mwanzoni mwa wiki hii baada ya matokeo duni yaliyoacha kikosi hicho katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa jedwali la Serie B.

Ranieri alipigwa kalamu na Watford mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 baada ya kuhudumu kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kipindi kisichozidi miezi minne.

Aliwahi kuongoza Leicester kutawazwa wafalme wa EPL mnamo 2015-16 baada ya kuwa kocha wa Chelsea na Fulham.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii