Waziri wa mambo ya kigeni wa Italy azuru Tunisia

Waziri wa mambo ya kigeni wa Italy Luigi Di Maio Jumanne wakati akiwa ziarani Tunisia, ameshauriana na rais Kais Saied kuhusiana na suala la wahamiaji wanaofanya safari hatari kuelekea Ulaya wakitafuta maisha mema.

Hiyo ni ziara ya kwanza ya DiMaio tangu Saied kujitwika madaraka yote Julai 25. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa afisi ya rais imesema kwamba Di Luigi amesifu juhudi zinazofanywa na selikali ya Tunisia katika kudhibiti tatizo la wahamiaji. 

Wakati wa kikao hicho, Saied aliangazia sheria za uhamiaji zilizopitwa na wakati akiongeza kwamba sheria mpya zinahitaji kubuniwa ili kuwapa wahamiaji haki zaidi pamoja na heshima. 

Mwezi Mei waziri wa mambo ya ndani wa Italy Luciana Lamorgese alitembelea Tunisia na kutangaza mkataba ambao ungetoa fedha kwa taifa hilo iwapo lingesitisha uhamiaji haramu kulekea Italy.

Di Maio pia alifanya mahojiano na asasi za kiraia wakati akiombwa majibu kutokana na kifo cha mhamiaji mmoja mwenye umri wa miaka 26 muda mfupi baada ya kuwasili kwenye kisiwa cha Sicily nchini Italy hapo Oktoba. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii