Kocha Nabi awakataa Fei Toto, Morrison

Kocha Mkuu wa Mabingwa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi ni kama amewakataa viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Bernard Morisson ambao wameshindwa kuripoti kambini kwa wakati.

Wawili hao tangu mwishoni mwa mwaka jana (2022) waliondoka kambini Young Africans, lakini kila mmoja amekua na sababu zake binafsi, ambazo zilifahamika kabla ya mambo mengine kuibuka.

Kocha Nabi ametoa kauli tata ambayo dhahir inawalenga Wachezaji hao, alipozungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu FC uliopigwa jana Jumatatu (Januari 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia alisema hapendezwi na tabia ya utovu wa nidhamu na siku zote mchezaji mwenye tabia hiyo hawezi kumpa kipaumbele cha kumtumia kwenye kikosi chake, ambacho kinaendelea kupata matokeo mazuri.


“Hakuna mchezaji mkubwa kuliko timu, sihitaji wachezaji ambao hawana nidhamu ndani ya timu na nimewaambia viongozi wasiingilie maamuzi yangu.”

“Fiston Mayele ni mchezaji ambaye anajituma na ana nidhamu, Mayele kila siku anawahi mazoezini na hata alipopewa mapumziko bado aliwahi kurudi mapema na kuungana na wenzake.”

“Sasa nahitaji wachezaji kama hao ambao watakuwa na nidhamu, sijali hata mchezaji anapendwa sana na mashabiki hata kama awe anafahamu sana mpira bado kama hana nidhamu sitaweza kumtumia katika timu, nitawatumia wachezaji wenye nidhamu kwa faida ya timu.” alisema Nabi


Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ amekua nje ya kikosi cha Young Africans licha ya kutakiwa kurudi Kambini, kufuatia sakata lake la kuvunja mkataba na Klabu hiyo.

Kwa upande wa Morrison, bado yupo nchini kwao Ghana ambako alikwenda kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya kifamilia mwishoni mwa mwaka jana (2022).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii