Mzozo wa kisiasa kati ya viongozi wawili wa juu wa Somalia ulizidi kuwa mbaya Jumatatu wakati Rais Mohamed Abdullahi Mohamed alipotangaza kwamba anamsimamisha kazi Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble.
Msemaji wa Rais Mohamed, maarufu Farmajo, alisema rais alichukua hatua hiyo kutokana na uchunguzi wa ununuzi haramu wa ardhi ya umma unaomhusisha Waziri Mkuu Roble. Kusimamishwa kwa Roble kunakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu kumshutumu Mohamed kwa njama katika uchaguzi wa bunge.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba vikosi vya usalama vimepelekwa kuzunguka ofisi za Roble, ambapo waziri mdogo wa habari nchini humo anaelezea kama mapinduzi yasiyo ya moja kwa moja. Viongozi hao wanaozozana walikuwa wamefikia makubaliano mapema mwaka huu ambayo yangeruhusu wajumbe 101 kuchagua wabunge ambao wangemchagua mkuu wan chi ajaye.
Waangalizi wanaonya ugomvi kati ya Farmajo na Roble unaweza kuivuruga serikali kutokana na tishio linaloendelea kutoka kwa kundi la waasi wa al-Shabaab lenye uhusiano na al-Qaida ambalo linapigana na serikali kuu kwa nia ya kukamata madaraka na kuweka utawala wa sharia nchini Somalia ambayo imekuwa ikikumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa tangu kupinduliwa kwa diktekta wa zamani Mohamed Siad Barre mwaka 1991