Unapowazungumzia wasanii wanaofanya vizuri kwa namna wanavyoigiza na kuuvaa uhusika kwa sasa, huwezi kuacha kumtaja Godliver Gordian, maarufu Anna wa ‘Juakali’.
Godliver ni mshindi wa kwanza wa tuzo za filamu zilizotolewa hivi karibuni mjini Mbeya katika kipengele cha mwigizaji bora wa kike, akiwabwaga aliokuwa akishindana nao, wakiwamo Christina Mroni, Tishi Abdallah na Johari Thabiti.
Alipata tuzo hiyo kupitia filamu ya ‘Juakali’, kwa waliotazama filamu hiyo hawakuwa na maswali walipoona aliyeshinda ni yeye.
Hilo lilionekana katika mitandao ya kijamii ambako kuliwekwa picha mbalimbali za kumpongeza, zikiwamo alizoshika tuzo hiyo, wengi wa walioona walisema alistahili kushinda. Tofauti na tuzo nyingine zinazofanyika nchini, tuzo hii haikuwa na malalamiko kutoka kwa mashabiki, kuashiria kuwa mwigizaji huyu alistahili.
“Hii siyo tuzo ya kwanza, mwaka 2019 nilipata tuzo ZIFF, kupitia filamu iitwayo ‘Aisha’ iliyoandaliwa na Kijani Production,” hayo ni maneno ya Godliver Goardian anapoanza kuelezea amani ya moyo anayopata msanii anapopata tuzo.
Anasema amefarijika sana kupata tuzo iliyoandaliwa na Serikali kwa sababu hata zile za ZIFF ni za kimataifa ingawa zinafanyika nchini.
“Tuzo ni kuthaminiwa, kwa awamu mbili mfululizo wasanii wametumika sana kwenye kampeni mbalimbali, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa ameliona hilo na kutukumbuka kwa kuwapo tuzo hizi, naishukuru wizara na Bodi ya filamu ambao wamelisimamia hili,” anasema Godliver.
Anasema kuwapo kwa tuzo kutaondoa dhana mbaya kwa watu kuwa wakishindwa kazi nyingine wanakimbilia katika sanaa, hasa uigizaji wakiamini ni kuongea ongea tu.
“Tuzo zitaleta ushindani wa kweli na kila atakayeingia huko atajipanga na kuichukulia kama kazi badala ya kuona ni eneo la kukimbilia walioshindwa kazi nyingine,” anasema.
Uigizaji wake
Anasema kuna sini hata yeye huwa zinamshangaza. “Nitolee mfano nilipopata ugonjwa wa afya ya akili, yale majina niliyokuwa nawaita wanaokuja kuniona hayakuwemo kwenye sini, mfano Love nilimuita Bombadier...ule ni ubunifu wangu mwenyewe.
“Ila hakuna sini rahisi kwangu, kila ninayopewa ni ngumu hata nikiambiwa nitazungumza na mtu koridoni, nitajiandaa kama nimeambiwa niigize mapigano, naamini hii ndiyo siri ya mafanikio, sina sini (nafasi ya uhusika wake katika filamu au kipande anachoigiza) nyepesi wala ngumu zote najipanga,” anasema Godliver.
Anasema pia hujipima kwa kuangalia kazi zake. “Kipaji nimeshajijua ninacho, ili kuona kama kinapanda au kushuka huwa naangalia kazi nilizozifanya, ninaweza kusema shabiki wa kwanza wa kazi zangu ni mimi mwenyewe.
“Naziangalia kujipima, hakika kadri siku zinavyokwenda ninazidi kuona nabadilika, tena kwa haraka, pia najitahidi nisimpe kazi muandaaji, mahali panapohitaji ubunifu ninauweka na ninafurahi unakubalika,” anasema.
Aliwezaje kuigiza kuumwa ugonjwa wa afya ya akili?
Anasema kwanza kabisa ni msanii ambaye hachagui sini, pia mtayarishaji wa filamu ya Jua kali, Lamata Mwendamseke alimpeleka mpaka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ambako aliwaona wagonjwa na kupata mawili matatu kutoka kwa wataalamu.
“Kuona, kusikia suala moja, kuwasilisha ni suala lingine. Kwanza kichwani ninajua ndugu, jamaa wanaoishi na wagonjwa wa aina hiyo wananiangalia, hivyo natakiwa niuvae uhusika kisawa, ilikuwa changamoto kidogo, lakini nashukuru nikitazama naona ninafanya vizuri,” anasema nyota huyo wa filamu.
Anaizungumziaje tasnia ya filamu?
Anasema kulikuwa na dhana kuwa imeshuka, lakini kiuhalisia haikuwahi kushuka bali ilisimama kwa muda.
Anasema kulikuwa na mabadiliko ya hapa na pale, hususan ujio wa tamthilia ambao uliondoa hamu ya mashabiki kununua filamu, pia kuona walichokizoea.
“Kupatikana vituo vya matangazo vinavyotoa fursa kuonekana filamu za nyumbani kumeamsha hamasa ya mashabiki kupenda kazi za nyumbani,” anasema.
Anasema kizuri zaidi wakati huu na vifaa vipo vya kutosha na wataalamu wa kazi za sanaa.
“Kwa mfano Jua Kali imeshinda kwa kuzingatia vitu vingi, vinajumuisha idara nyingi, ikiwamo ‘Art Department’ ambayo jukumu lake ni kuangalia sini gani inaigizwa katika mazingira yapi, inahitaji uhalisia.
“Jua Kali inatumia rangi ya kijani hivyo kuhakikisha kwa namna yoyote inakuwepo, pia kuna idara ya mavazi, mapambo, taa na kamera ilimradi kila mmoja anafanya eneo lake na kwa usahihi, hii inaleta hamu ya tamthilia husika kutazamwa bila mtazamaji kuchoka,” anasema.
Anatazama kazi za wengine?
Godliver anasema anatazama kazi za filamu za wasanii wa Hollywood na nyumbani kuona wengine wanafanya nini. “Sizitazami kujifunza bali nazitazama kisha namtafuta Godliver au Anna wa Juakali kwa sababu sitaki kuwa kama fulani nataka kuwa mimi.
“Nawaangalia waigizaji wengi wa Hollywood akiwamo Viola Devis, Meghan, Gabriela, wapo wengi nimewataja hao haraka haraka,” anamalizia Godliver.
Kuna faida kufanya utafiti kabla ya kuigiza?
Zipo faida nyingi siyo moja, hasa kwa sini tofauti kidogo, siyo za kuwasilisha kwa kuzungumza bali kwa vitendo.
Ukifanya utafiti japo kidogo utajua hicho unachokiigiza au watu unaoigiza huwa wanafanya nini.
“Nilieleza hapo juu kuwa kabla ya kuigiza ugonjwa wa afya ya akili, nilikwenda Mirembe kufanya utafiti kidogo umenisaidia, kuongeza ubunifu ni kazi ya msanii, lakini utaongeza ubunifu kwa kitu unachokijua kidogo”.
Anasema huwezi kuigiza filamu ya utunzaji mazingira kama hujafanya utafiti, wasanii wakifanya tafiti ndogo wataigiza filamu nzuri zaidi.