Chama cha Biden chafanya vyema chaguzi za kati ya muhula

Chama cha Democratic kitadumisha udhibiti wa Bunge la Seneti nchini Amerika, baada ya kushinda kura muhimu katika jimbo la Nevada.

Hapo jana Jumapili, Seneta Catherine Cortez alitabiriwa kumshinda mpinzani wake, Adam Laxalt, aliyekuwa akiungwa mkono na aliyekuwa rais wa taifa hilo, Donald Trump.

Matokeo hayo ndiyo bora zaidi ya uchaguzi wa kati ya muhula kwa chama kilicho uongozini kwa miaka 20 iliyopita.

Rais Joe Biden alieleza kufurahishwa sana na matokeo hayo. Alisema ni wakati wa chama cha Republican “kuamua wao ni nani.”

Kiongozi wa Wengi wa Seneti wa Democratic, Chuck Schummer, alisema matokeo hayo yanaonyesha raia wa Amerika wameamua kukataa kile alitaja kuwa “propaganda za uwongo” zilizoenezwa na Republican.

Kufuatia hilo, chama cha Democratic kitakuwa na viti 50 katika Seneti huku Republican ikiwa na viti 49.

Jimbo la Georgia litashiriki duru ya pili ya uchaguzi huo mwezi Desemba. Katika hali ambapo vyama hivyo vitakuwa na idadi sawa ya viti, basi Makamu wa Rais Kamala Harris atalazimika kupiga kura.

Hata hivyo, Republican inatabiriwa kuchukua udhibiti wa Bunge la Wawakilishi, kulingana na matokeo yaliyohesabiwa kutoka wilaya kadhaa. Uchaguzi huo ulifanyika Jumanne iliyopita.

Ikiwa Republican itachukua udhibiti wa bunge hilo, basi huenda kikavuruga ajenda kubwa ya maendeleo ya Rais Biden.

“Sijashangazwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo. Hilo linaonyesha ubora wa wawaniaji wetu,” akasema Rais Biden akiwa nchini Cambodia, anakohudhuria kikao maalum.

Wakati huo huo, watu wawili walifariki Jumamosi baada ya ndege mbili za kijeshi zilizokuwa zikishiriki kwenye maonyesho ya ndege katika eneo la Dallas, Texas, kugongana zikiwa hewani


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii