Qatar yaaga mapema michuano ya Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya Qatar imekuwa ya kwanza kuaga mashindano ya kombe la dunia baada ya kufungwa na Senegal bao 3-1 siku ya Ijumaa katika uwanja wa  Al Thumama Doha Qatar.

Timu hiyo imeaga mapema kuliko ilivyotarajiwa na uweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutolewa kwenye michuano hiyo huku wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi.Mabao ya Senegal-Simba wa Teranga yalifungwa na Boulaye Dia, Famara Diedhiou na Bamba Dieng.

Senegal wanahitaji hata hivyo kushinda mechi yao ya mwisho na Ecuador ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika raundi ya 16 ya michuano hii.

Senegal imekuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kupata ushindi katika michuano hii.

Kwa upande wake Uholanzi na Ecuador wapo katika nafasi nzuri ya kuweza kusonga mbele kwa kuwa kila mmoja wao wana pointi 4.

Nao Vijana wa Marekani walikutana na mahasimu wao Uingereza katika mchezo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu nchini Marekani na Uingereza ambapo wamarekani wakiwa katika sikukuu ya Thanksgiving walijazana kwenye baa mbali mbali kuangalia mchezo huo.

Timu ya Marekani ambayo ina vijana wengi wenye umri mdogo ikiongozwa na kapteni mwenye umri wa miaka 23 tu Tyler Adams ilipambana vikali na Uingereza timu ambayo imesheheni majina mengi makubwa katika kombe la dunia na kutoka nayo sare ya 0-0.

Marekani walifanya vyema dhidi ya timu nambari 5 duniani Uingereza, lakini hakuna timu iliyoweza kupata bao wakati timu hizo mbili zilipotoka sare ya 0-0 katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Dunia.

Nahodha wa kikosi cha Uingereza Harry Kane amesema amesikitika hawakufanya vizuri dhidi ya Marekani.

Marekani anahitaji ushindi kusonga mbele wakati Uingereza inahitaji droo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii