Kanye West Kugombea urais 2024

Rapa Kanye West amesema ana nia ya kugombea urais wa Marekani mwaka 2024, licha ya kukabiliwa na kashfa kadhaa kutokana na tabia yake ya hivi karibuni.

Nyota huyo ambaye amebadilisha jina lake kihalali na kuwa Ye, alituma video ya nembo yake ya kampeni kwenye mitandao ya kijamii, sambamba na nukuu ya Ye 24.

Pia alidai kuwa alimwomba Donald Trump kuwa mgombea mwenza wake.

Hapo awali West aliwania urais mwaka 2020, lakini kampeni hiyo haikufua dafu, na kupata kura 70,000.

Madai yake ya hivi karibuni yalikuja katika video iliyochapishwa baada ya West kuonekana katika kilabu cha gofu cha Trump cha Mar-A-Lago mapema wiki hii, akiandamana na Nick Fuentes, mzalendo mashuhuri wa kizungu.

West alisema ombi lake la mgombea mwenza lilimwacha rais huyo wa zamani, ambaye hivi majuzi alizindua kampeni yake ya kuchaguliwa tena, “likiwa na wasiwasi zaidi”.

Katika video iliyopewa jina la Mar-A-Lago Debrief, West alidai: “Trump kimsingi alianza kunizomea mezani, akiniambia nitashindwa.

Wakati West akiwania urais mwaka 2020, alitangaza kampeni yake akiwa amechelewa sana kujitokeza kwenye kura katika takribani majimbo sita.

Alifanya mkutano mmoja tu, ambapo aliangua kilio alipokuwa akizungumzia utoaji wa mimba, na kufadhili matangazo mawili ya televisheni.

Mwishowe, aliorodheshwa tu kama mgombea katika majimbo 12. Kwa ombi lake la 2024, mwanamuziki huyo alisema kuwa amemsajili mchambuzi wa mrengo wa kulia Milo Yiannopoulos kama meneja wake wa kampeni.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii