Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amemuongeza kwenye benchi lake, staa wa zamani wa Msimbazi, Mussa Hassan Mgosi.
Straika
huyo aliyekuwa anakochi timu ya vijana ya Simba, tayari ameanza kazi
yake rasmi na juzi alikuwa benchi Simba ikiivaa Mbeya City kwenye Uwanja
wa Sokoine.
Mgosi ambaye ni staa wa zamani wa Mtibwa na DC Motemba
Pembe ya DRC, amechukua nafasi ya Selemani Matola ambaye amekwenda
kwenye kozi ya ukocha Leseni A Diploma ya CAF inayoendelea kisiwani
Unguja, Zanzibar.
Licha ya Mgunda kutotaka kuingia kiundani lakini
habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema ndiye aliyemtaka
Mgosi sawa na viongozi ambao walikuwa wakimfikiria kama mbadala wa
Matola.
Baada ya Matola kuondoka, Mgunda ambaye ni kocha wa zamani wa
Coastal Union na Taifa Stars, aliongezewa kocha wa viungo na wa makipa
huku Mgunda akisubiri bosi wake ambaye Mwanaspoti linajua ni raia wa
Ureno atakayechukuwa nafasi ya Zoran Maki aliyetimka.
Mgosi anakaimu kwa muda wakati huu Matola yupo masomoni
ambapo kozi yake hiyo itakuwa ikifanyika kwa vipindi tofauti ndani ya
mwaka mmoja.
"Mgosi atakuwa anakaimu nafasi yake akiwa hayupo lakini
kozi yao ni ya siku chache akirudi anaendelea na majukumu yake kama
kawaida,"alidokeza mmoja wa viongozi wa Simba ambayo inafanya siri kubwa
suala la Kocha Mkuu licha ya kwamba taarifa za awali zilieleza alipaswa
kutua Jumatatu iliyopita.
Mgosi mbali ya kuitumikia Simba kwa
mafanikio makubwa kama mchezaji, baada ya kutundika daluga aliaminiwa na
kupewa timu ya wanawake akiipa mataji mawili na baadae kupewa jukumu la
kuwa kocha wa timu ya vijana 'Simba B'.
Uongozi wa Simba ndio
uliogharamia kozi ya Matola huku ikipanga kuwaendeleza nyota wao
walioipa timu mafanikio baada ya kuacha kucheza akiwemo Erasto Nyoni na
Nahodha John Bocco.