Ufaransa waanza kutetea ufalme wao kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Australia

Mabingwa  watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa, walianza kampeni za kipute hicho mwaka huu kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Australia katika pambano la Kundi D lililochezewa ugani Al Janoub.

Licha ya kukosa huduma za wanasoka nyota akiwemo fowadi Karim Benzema ambaye ni mchezaji bora zaidi duniani, Ufaransa waliteremkia wapinzani wao na kuwalemea katika kila idara.

Ingawa Craig Goodwin aliwaweka Australia kifua mbele kunako dakika ya tisa, Ufaransa walisawazisha kupitia Adrien Rabiot kabla ya mabao mengine kujazwa kimiani na Kylian Mbappe na Olivier Giroud aliyecheka na wavu mara mbili.

Giroud aliyejaza kikamilifu pengo la Benzema – mshindi wa taji la Ballon d’Or aliyepata jeraha la paja akiwa kambi ya mazoezi nchini Qatar – alikuwa mwiba kwa mabeki wa Australia.

Wanasoka wengine wa Ufaransa ambao walihangaisha pakubwa madifenda wa Australia ni Ousmane Dembele, Kingsley Coman na Antoine Griezmann.

Mabao mawili yalifungwa na Giroud yalimwezesha kufikia rekodi ya Thierry Henry – mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Ufaransa kwa magoli 51. Sasa Giroud ambaye ni mshambuliaji wa AC Milan, ana fursa ya kuvunja rekodi hiyo kwenye kampeni za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Qatar.

Zaidi ya kukosa huduma za Benzema, kocha Didier Deschamps alikuwa pia bila maarifa ya beki Presnel Kimpembe, viungo N’Golo Kante na Paul Pogba pamoja na mvamizi Christopher Nkunku.

Miamba hao waliopepeta Croatia 4-2 katika fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, pia walipata pigo la kumpoteza beki Lucas Hernandez aliyepata jeraha katika dakika ya tisa ya mchezo.

Ushindi wa Ufaransa uliwakweza kileleni mwa Kundi D kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Denmark na Tunisia walioambulia sare tasa katika mechi nyingine ya kundi hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii