Tunisia wasema wako tayari kwa mtihani wa Denmark katika Kundi D

TUNISIA almaarufu Carthage Eagles watafungua kampeni za Kombe la Dunia kwa kibarua kizito dhidi ya Denmark katika uga wa Education City mjini Al Rayyan.

Wawakilishi hao wa Afrika wana rekodi duni ya kupoteza mechi tisa kati ya 15 kwenye fainali tano zilizopita za Kombe la Dunia. Rekodi hiyo inawaweka nyuma ya Australia na Saudi Arabia ambao wamepigwa mara 11 kutokana na mechi 16. Australia wamepoteza michuano 10 kati ya 16 iliyopita kwenye kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia.

Hofu zaidi kwa Tunisia ni ubovu wa rekodi yao dhidi ya vikosi kutoka bara Ulaya. Wafalme hao wa Afrika 2004 walipoteza mechi nne zilizopita za Kombe la Dunia dhidi ya Uhispania na Ukraine mnamo 2006 kabla ya Uingereza na Ubelgiji kuwazamisha 2018.

Makala ya Qatar ni ya sita kwa Tunisia kunogesha. Kikosi hicho kinachoshikilia nafasi ya 30 duniani, hakiwajawahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi kwenye makala yote matano ya awali katika Kombe la Dunia. Ndicho kikosi ‘dhaifu’ zaidi miongoni mwa mataifa matano (mengine yakiwa Senegal, Ghana, Morocco na Cameroon) yanayowakilisha Afrika nchini Qatar.

Mnamo 1978, Tunisia waliweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza kutoka Afrika kuwahi kushinda mechi ya Kombe la Dunia kwa kupepeta Mexico 3-1 nchini Argentina. Tangu wakati huo, wameshinda mechi moja pekee kati ya 14 kwenye mashindano hayo – walikomoa Panama 2-1 mnamo 2018 nchini Urusi.

Masogora hao wa mkufunzi Jalel Kadri walifungua kampeni zilizopita za Kombe la Dunia nchini Urusi kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Uingereza kabla ya Ubelgiji kuwacharaza 5-2 katika mchuano wa pili. Baada ya kuvaana na Denmark, wataonana na Australia mnamo Novemba 26, siku tatu kabla ya kukwaruza na Ufaransa.

“Japo tuna rekodi mbovu, nina imani tele kwa kikosi changu. Tutajitahidi kadri ya uwezo kukabiliana na kibarua kizito kinachotusubiri,” akasema Kadri kwa kusisitiza kuwa wanalenga kulaza Denmark na Australia ili kupata motisha ya kumenyana na Ufaransa mwishowe.

Huku Tunisia wakitegemea zaidi maarifa ya vigogo Youssef Msakni, Ali Maaloul na Wahbi Khazri, tegemeo la Denmark ni kipa Kasper Schmeichel (Nice) na viungo Christian Eriksen (Man-United na Pierre-Emile Hojbjerg (Tottenham).

Nahodha wa Tunisia, Wahbi Khazri, amesema kikosi chao kina ubora utakaokiwezesha kutamba dhidi ya Denmark kwa kukiri kuwa mechi ya kirafiki iliyoshuhudia mabingwa mara tano wa dunia, Brazil, wakiwaponda 5-1 mnamo Septemba 2022 ilikuwa kipimo halisi cha uthabiti wao na jukwaa zuri “lililowafundisha mengi” kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Qatar kupulizwa.

Tunisia walipimana nguvu na Brazil mnamo Septemba 27 jijini Paris, baada ya kulaza Comoros 1-0 mnamo Septemba 22 mjini Orleans, Ufaransa.

“Tumekabiliana na masogora wa kiwango cha juu zaidi kimataifa na tukajipima nguvu dhidi ya miamba. Tuliona tulichokosa na tukaboresha katika maandalizi yetu,” akasema Khazri anayechezea Montpellier ya Ufaransa.

“Tuna uwezo wa kucheza dhidi ya timu kubwa. Ndoto yetu mwaka huu ni kutinga raundi ya muondoano,” akasisitiza Khazri aliyeongoza Tunisia kuzoa taji la Kirin Cup mnamo Juni baada ya kutandika Chile 2-0 na kulaza Japan 3-0.

Sogora huyo aliwahi pia kuongoza Tunisia kudengua Nigeria kwenye hatua ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) mwaka huu wa 2022 kabla ya Burkina Faso kuwang’oa kwenye robo-fainali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii