Mazrui augua Uviko-19

Waziri wa Afya, Ustawi wa jamii, Wazee, Jinsia na Watoto,  Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amepata maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 lakini hali anaendelea vizuri.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mazrui amesema alibainika kuwa na ugonjwa huo juzi Desemba 24 baada ya kwenda kupimwa hospitalini.

“Siku ya Alhamisi nilianza kujisikia homa kali mafua, kuharisha nilienda hospitali kupima nikakutwa na maabukizi kwahiyo kwasasa nimejitenga nyumbani siendi kazini mpaka kipindi cha wiki moja niangalie hali itakavyokuwa,” amesema

Amesema hata mtu akienda kumtembelea nyumbani kwake kwa sasa wanaongelea dirishani ili kuepusha kusambaza maambukizi ya ugonjwa huo.

Amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote dhidi ya ugonjwa huo na kuchanja akidai kwamba chanjo ndio imemsaidia kupunguza ukali wa ugonjwa huo

“Ugonjwa upo na watu wanaumwa lakini hawaendi hospitali kupimwa na kupata matibabu, wengi wanabaki nyumbani na kujitibu wenyewe, tutoke twende hospitalini, lakini wananchi waendelee kunawa mikono kuvaa barakoa na kuacha mikusanyiko isiyo ya lazima,” amesmea na kuongeza

"Mimi kuchanja kumenisaidia sana kwahiyo wachanje wasipuuze, mtu akipata inampunguzia makali."

Juzi Desemba 24, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazimmoja Dk Marijani Msafiri alisema kwatu 89 wakiwemo wafanyaakzi wa hopsitali hiyo 38 wamegundulika kuwa na ugonjwa wa huo ndani ya kipindi cha wiki moja.

Alisema wagonjwa hao ni kati ya wagonjwa 143 waliofanyiwa kipimo cha Uviko 19 kuanzia Desemba 16 mwaka huu hadi Desemba 24.

Aidha alisema katika wafanyakazi hao hakuna hata mmoja aliyelazwa maana hawana dalili kubwa za kulazwa bali wanaendelea na matibabu na kupewa mapumziko ya muda mfupi kulingana na hali zao.

Kati ya wagonjwa 51, ni wagonjwa tisa tu waliolazwa, wengi wao hawana ugonjwa wa kuhatarisha maisha ya uhitaji wa kulazwa na badala yake wanapatiwa matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani na kufuata taratibu za kujikinga na ugonjwa huo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii