Bomu lalipuka katika mkahawa uliojaa watu siku ya Krismasi - DRC CONGO

Maafisa nchini DR Congo wanasema kwamba takriban watu sita wamefariki katika shambulio la mlipuaji wa kujitoa muhanga katika makahawa uliojaa watu katika mji wa mashariki wa Beni.

Maafisa wa polisi walimzuia mlipuaji huyo kuingia katika jumba hilo , lakini akajilipua katika lango la mkahawa huo na kujiuwa pamoja na watu wengine watano.

Watu wengine 13 walijeruhiwa. Maafisa walilaumu wapiganaji wa ADF - kundi linaloshirikishwa na kundi la Islamic State{ IS} kwa kutekeleza shambulio hilo .

Kufikia sasa hakuna kundi lolote lililokiri kutekeleza shambulio hilo. Zaidi ya watu 30 walikuwa wakisherehekea siku kuu ya Krismasi katika mkahawa wa Box Restaurant wakati bomu hilo lilipolipuka , mashahidi wawili waliambia AFP.

Kulikuwa na watoto na maafisa wa utawala wa eneo hilo wakati wa tukio hilo.

''Nilikuwa nimekaa pal''e alisema mtangazaji mmoja wa kituo cha redio katika eneo hilo Nicolas Ekila akizungumza na kituo cha habari cha AFP. 

''Kulikuwa na pikipiki iliokuwa imeegeshwa pale, mara pikipiki hiyo ikaondoka ghafla na baadaye nikasikia sauti kubwa''.

Baada ya mlipuko huo, afisa wa jeshi anayesimamia shughuli za dharura katika eneo la mashariki nchini humo aliambia wakaazi kurudi nyumbani kwa usalama wao wenyewe.

Kumekuwa na ghasia za mara kwa mara katika eneo la Beni kati ya wanajeshi na wapiganaji wa Kiislamu katika wiki za hivi karibuni.

Mwezi Novemba , wnajeshi wa DRC wakishirikiana na wale wa Uganda walianzisha operesheni dhidi ya wapiganaji wa ADF katika jaribio la kumaliza msururu wa mashambulizi mabaya.

Utawala nchini Uganda unasema kwamba kundi hilo ndilo lililohusika na mashambulizi ya hivi karibuni nchini humo , ikiwemo lile la mjini Kampala.

Kundi hilo lilianzishwa mwaka 1990 na Waganda ambao hawakupendelea jinsi serikali ya taifa hilo ilivyokuwa ikiwafanyia Waislamu , lakini lilifukuzwa na wafuasi wake wakatoroka na kuvuka mpaka na kuingia nchini DR Congo.

Lilianzisha makao yake mapya mashariki mwa DR Congo na limelaumiwa kwa mauaji ya raia wengi katika eneo hilo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, ikiwemo mashambulizi dhidi ya raia Wakristo. 

Mnamo mwezi Machi , Marekani ililiorodhesha kundi hilo katika orodha yake ya makundi ya ugaidi yanayohusishwa na IS. 

Kwa upande wake IS linasema kwamba ADF ni mshirika wake .

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii