Wabunge nchini Iraq jana walimchagua Abdul Latif Rashid, mwanasiasa mkurdi mwenye umri wa miaka 78 kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Afisa mmoja wa bunge amesema kuwa Rashid alipata zaidi ya kura 160 dhidi ya 99 za Barham Saleh anayemaliza muda wake uongozini.
Rashid mara moja alimchagua Mohammed Shia al-Sudani, mwanasiasa wa Kishia kama waziri mkuu mteule, kwa matumaini ya kumaliza mwaka mmoja wa migogoro ya kisiasa na ghasia katika taifa hilo lililokumbwa na vita, huku akimtwika jukumu la kupatanisha makundi yanayohasimiana ya Kishia na kuunda serikali mwaka mzima baada ya Iraq kupiga kura mara ya mwisho.
Sudani, ambaye anaungwa mkono na vikundi vyenye ushawishi vinavyoiunga mkono Iran, aliapa kuunda serikali haraka iwezekanavyo. Sasa ana siku 30 kuunda serikali mpya yenye uwezo wa kuwa na viti vingi bungeni.