Rais wa Uganda Yoweri Museveni amejitetea kwa hatua yake ya kumpandisha cheo mwanawe Jenerali Muhoozi Kainerugaba licha ya kumtimua kama kamanda wa wanajeshi wa ardhini wa Uganda.
Katika mageuzi yaliyofanywa Jumanne, Oktoba 4, Museveni alimteua Jenerali Kayanja Muhanga kuwa kamanda mpya wa majeshi ya ardhini ya Uganda na kuchukua nafasi ya Muhoozi.
Mageuzi haya yalitokana na jumbe za Muhoozi kwenye mtandao wa Twitter ambapo alisema kuwa anahitaji chini ya wiki mbili kuvamia na kuteka jiji la Nairobi.
Hata hivyo umma uliuliza maswali ya alichowaza Museveni kwa kumpandisha cheo Muhoozi ambaye alikuwa ‘ameadhibiwa’ kwa jumbe zake za kivita kuhusu nchini jirani.
Kupitia kwa taarifa hata hivyo, Museveni ametetea hatua yake akisema kuwa licha ya jumbe hizo, kuna mengi ambayo Muhoozi amefanyia Uganda na hayawezi kufutwa kwa kosa moja.
“Lakini mbona kumpandisha cheo na kuwa Jenerali kamili baada ya jumbe hizi? Hii ni kwa sababu hii ni mara moja tu ambayo amekosa kama mtumishi wa umma. Kuna mambo mengine mazuri ambayo Jenerali amefanya na bado anaweza kufanya,” Museveni alisema.