Watu watatu wamekufa katika ujenzi wa viwanja Qatar

Shirikisho la soka duniani FIFA limesema watu watatu wamekufa katika miaka ya hivi karibuni katika maeneo ya ujenzi wa viwanja vitakavyotumiwa kwa ajili ya mechi za kombe la dunia nchini Qatar.

FIFA imelielezea shirika la habari la dpa kuwa watu wengine 37 walipoteza maisha yao japo vifo hivyo havikutokea katika maeneo ya ujenzi wa viwanja na kwamba havikuwa na uhusiano wowote na kazi ya kamati ya maandalizi ya FIFA.

Qatar imekuwa ikikosolewa juu ya jinsi inavyoshughulikia wafanyikazi wa kigeni nchini humo. Gazeti la The Guardian la nchini Uingereza liliripoti mwaka uliopita kuwa maelfu ya wafanyikazi kutoka mataifa ya Asia walikufa nchini Qatar. Kombe la dunia la FIFA la mwaka 2022 litaandaliwa nchini Qatar kuanzia Novemba 20 hadi Disemba 18.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii