Mwili wa Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Paul Rupia anatarajiwa kuzikwa Ijumaa hii ya Septemba 23, 2022 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Balozi Rupia alifariki dunia Septemba 16, 2022 huko Afrika Kusini na mwili wake unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo mchana Jumatano ambapo utapokelewa na wanafamilia wakiongozwa na mjane, Rose Rupia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu, Simon Rupia, mwili utawasili leo nchini na unatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni Ijumaa Septemba 23, 2022.
"Kabla ya maziko, kutakuwa na misa ya kumwombea kwa Mungu katika Kanisa Kuu la Anglikana la Mtakatifu Albano na kufuatiwa na sherehe za uhai wake katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
"Atakumbukwa sana na mke wake, Rose Rupia, watoto wake, wakwe zake, wajukuu, familia na marafiki," ameeleza Simon katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Mazishi ya Balozi Rupia yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wanafamilia katika kumsindikiza mpendwa wao katika safari yake ya mwisho.
Balozi Rupia alizaliwa Januari 7, 1936 katika Hospitali ya Nkolandoto, Shinyanga akiwa mtoto wa pili wa Mzee John Rupia.
Balozi Rupia alipata elimu yake ya msingi katika Chuo cha Mtakatifu Andrew, Minaki na baadaye alijiunga na shule ya Sekondari ya The Aga Khan ya jijini Dar es Salaam.
Baada ya hapo aliendelea na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Cuttington nchini Liberia na kuhitimu shahada ya sanaa katika Sayansi ya Siasa.
Taarifa ya familia inaeleza baada ya hapo, alisomea shahada yake ya uzamili katika Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha New York (NYU) nchini Marekani.
Kuanzia mwaka 1963, Balozi Rupia alianza taaluma yake katika utumishi wa umma kwa kujiunga na Wizara ya Mambo ya Nje ambako alidumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 23.
Alihudumu katika wizara hiyo katika nyadhifa mbalimbali kuanzia ofisa utumishi wa mambo ya nje, mkuu wa mabalozi, na hatimaye kama Katibu Mkuu kwa miaka miwili ya mwisho ya utumishi wake katika wizara hiyo.
Baada ya hapo, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, kuhudumu katika serikali yake kama Katibu Mkuu Kiongozi kuanzia 1986 - 1995.
Baada ya kustaafu utumishi wa umma, Balozi Rupia alikwenda kugombea ubunge katika jimbo la Ukonga na kuchaguliwa kuwa mbunge kuanzia mwaka 1995 - 2000.
Balozi Rupia amefanya kazi kwenye bodi nyingi na kamati maalum katika taasisi tofauti kuanzia elimu, kanisa, na benki.
Atakumbukwa daima kwa mchango wake wa kupigiwa mfano kwa nchi na pia taaluma yake iliyotukuka akiwa mtumishi wa umma na mwanadiplomasia.