Ethiopia yaikataa ripoti ya Umoja wa Mataifa

Ethiopia imeikataa ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanaoituhumu kwa uwezekano wa kuendelea kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika eneo linalokabiliwa na vita la Tigray, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa njaa kama silaha ya vita. Tume ya wataalamu wa haki za binadamu kuhusu Ethiopia imesema imegundua ushahidi wa ukiukaji mpana wa haki za binadamu unaofanywa na pande zote katika vita hivyo tangu mapigano yalipozuka Tigray karibu miaka miwili iliyopita. Mwenyekiti wa tume hiyo Kaari Betty Murungi amesema kunyimwa chakula, dawa na huduma za msingi kunasababisha athari kubwa kwa watu wa Tigray. Mjumbe wa kudumu wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva Zenebe Kebede amesema tume hiyo imechochewa kisiasa na tathmini yake ya mwisho inakinzana na ina upendeleo akidokeza kuwa wataalamu hawakuzingatia ukatili uliofanywa na wapiganaji wa jeshi la ukombozi la watu wa Tigray TPLF.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii