Balozi Rupia afariki dunia

 Katibu Mkuu Kiongozi wa tano, Balozi Paul Rupia amefariki dunia leo asubuhi nchini Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 84.

Taarifa ya kifo chake imetolewa leo Septemba 16 kwa Mwananchi na mtu wa karibu na familia hiyo, Mzee wa Atikali ambaye naye alipewa taarifa hiyo na mtoto wa marehemu, Peter.

Mbali na wadhifa wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Rupia amekuwa ofisa katika Wizara ya Mambo ya Nje kuanzia mwaka 1963 na baadaye alikuwa balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali ikiwamo Uingereza na baadaye balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Pia, aliwahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Watu wa Dar es Salaam.

Balozi Rupia aliyezaliwa Januari 21, 1938 katika hospitali ya Nkolandoto mkoani Shinyanga ni mtoto wa mpigania uhuru, mfanyabiashara na mwanasiasa, John Rupia.

Kwa nyakati tofauti, (Baba yake) John Rupia amekuwa mwaasisi wa chama cha TAA (Tanganyika African Association), TANU, (Tanganyika African National Union) na AA (African Association (AA) na alishiriki katika baraza maarufu la wazee wa TANU wakati huo akiwa pamoja na kina Mzee Mwinyikambi, Tambaza, Mshume, Chamwenyewe, Haidar Mwinyimvua na Rajab Diwani.

Na walipotoka TAA na kuanzisha TANU, John Rupia alipewa nafasi ya kuwa Makamu Mwenyekiti chini ya uongozi wa Julius Nyerere, akiwa na kadi namba 7.

Baba yake balozi Rupia (John Rupia) anatajwa kuwa ndiye aliyekuwa mfadhili namba moja kwa kukiendesha na kukikuza chama cha TANU kwa kujitolea kulipa mishahara na posho.

Pia, kwa sehemu kubwa aligharamia safari ya Mwalimu Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kuelezea dunia kwamba Watanganyika walikuwa tayari kujitawala.

Baba yake balozi Rupia ndiye alimnunulia suti za kuvaa safarini na kumpa fedha za kujikimu Mwalimu Nyerere katika safari yake nchini Marekani.

Balozi Rupia ameacha mjane Rose Rupia na watoto Peter, Suzan, Pauline na Simon.

Makatibu wakuu kiongozi waliopita

    Dunstan A. Omary 1962- 1964

    Joseph A. Namata 1964-1967

    Dickson A. Nkembo 1967-1974

    Timothy Apiyo 1974-1986

    Paul M. Rupia 1986-1995

    Martene Y.C Lumbanga 1995-2006

    Philimon L. Luhanjo 2006-2011

    Ombeni Sefue 2012-2016 [3]

    John William Kijazi 2016-2021

    Bashiru Ally 2021-2021

    Hussein Athuman Kattanga 2021

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii