Baada ya kuapishwa, rais wa Angola aahidi ajira kwa vijana

Rais wa Angola Joao Lourenco, Alhamisi aliahidi nafasi za kazi kwa vijana wa nchi hiyo, ambao haki zao zimekandamizwa, huku wengi wao wakiwa hawana ajira.

Laurenco alitoa ahadi hiyo alipopishwa baada ya uchaguzi ambao aliokiri kuwa ulipingwa vikali na upinzani.

Mahakama ya Katiba ya Angola ilitupilia mbali malalamshi yaliyowasilishwa na chama cha upinzani, UNITA, kilichoshindwa katika uchaguzi wa Agosti 24.

UNITA, kundi la zamani la waasi ambalo lilipigana na chama tawala cha MPLA, kwa takriban miongo mitatu, lilipata kura zake nyingi kutoka kwa vijana wanaohisi kutengwa na utajiri wa mafuta nchini humo.

Wachambuzi wanahofia ghadhabu zao zinaweza kugeuka kuwa ghasia, iwapo wataitikia wito wa UNITA, wa maandamano kuanzia Septemba 24.

Usalama ulikuwa umeimarishwa si haba katika mji mkuu wa Angola, Luanda, jana Alhamisi, na UNITA, ambayo viongozi wake hawakuhudhuria hafla hiyo, ilishutumu kuwepo kwa maafisa wengi wa polisi, kama juhudi za kukabiliana na uwezekano wa maandamano.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii