Wakenya Waambiwa Wawe Tayari Kuumia

Muungano wa Watengenezaji Bidhaa (KAM) umewataka Wakenya kujiandaa kwa hali ngumu zaidi ya maisha.

Kulingana na KAM, bei ya bidhaa nyingi muhimu itapanda kwa kiasi kikubwa wakati wowote kuanzia sasa. Mkuu wa Sera na Utafiti wa KAM, Job Wanjohi, kuwa kupandishwa kwa bei ya mafuta na umeme kumesababisha gharama ya uzalishaji wa bidhaa kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Bei ya mafuta imeongezeka na kufikia kiwango cha kuvunja rekodi. Bei ya umeme nayo imeongezeka licha ya serikali kuahidi kuipunguza kwa asilimia 15. Sarafu ya Kenya nayo inaendelea kudorora dhidi ya Dola ya Amerika. Masuala haya yamesababisha gharama ya kutengeneza bidhaa kuongezeka. Mwananchi ndiye ataumia zaidi kutokana na kupanda kwa gharama ya uzalishaji,” anasema Bw Wanjohi.

Watengenezaji wa bidhaa sasa wanataka serikali kupunguza ushuru unaotozwa mafuta ili kuwakinga raia dhidi ya kulemewa na gharama ya juu ya maisha.

“Serikali ipunguze ushuru unaotozwa mafuta kama njia mojawapo ya kushusha bei ya bidhaa hiyo. Hii itawakinga Wakenya dhidi ya kulemewa na bei ya juu ya bidhaa muhimu kama vile chakula,” akasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kusaga unga ya Capwell Industries Ltd, Rajan Shah naye alionya kuwa bei ya unga huenda ikapanda zaidi ndani ya siku chache zijazo kufuatia ongezeko la gharama ya umeme na mafuta.

“Viwanda vinatumia kiasi kikubwa cha umeme na mafuta kusaga mahindi na nafaka nyinginezo. Vilevile, gharama ya kusafirisha unga hadi madukani kote nchini imeongezeka. Hivyo, mwananchi ataumia zaidi,” akasema Bw Rajan.

Kwa sasa unga wa mahindi unauzwa kwa bei ya wastani ya Sh210. Bidhaa zingine zinazotarajiwa kupanda bei ni mkate ambao unauzwa Sh60 kwa gramu 400, maziwa pakiti ya nusu lita Sh57 na mafuta ya kupikia lita moja Sh450.

Mnamo Jumatano bei ya mafuta ilipanda kwa zaidi ya Sh20 kwa kila lita huku ya stima nayo ikiongezeka kwa asilimia 15.7.

Nyongeza hizi ni kionjo tu kwani tayari Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) imetangaza itaongeza ushuru wa bidhaa zingine kuanzia Oktoba 1 kuambatana na mfumuko wa gharama ya maisha.

KRA ilipokuwa ikitangaza ushuru mpya nayo Tume ya Kusimamia Kawi na Petroli (EPRA) mbali na kutangaza nyongeza ya mafuta pia ilipandisha bei ya stima.

MAFUTA

Hii ina maana kuwa utakuwa ukipata vipimo 39.5 vya stima kwa Sh1,000 badala ya 45.7 vya awali.Wataalamu wanasema pia kuna uwezekano wa nauli kupanda kufuatia kuongezwa kwa bei ya dizeli.

Wenye magari ya kibinafsi nao watalazimika kugharimika zaidi kusafiri baada ya bei ya petroli kupanda kwa Sh20.18 kwa lita moja.

Wakenya wanaotegemea mafuta taa kupika ama kupata mwangaza nao wamegongwa kiboko bidhaa hiyo ilipoongezwa bei hadi Sh147.94 kwa lita moja.

Ongezeko hili linatarajiwa kuathiri zaidi wakazi wa maeneo ya mashambani na mitaa ya mabanda.

Wanaotumia gesi kupikia pia hawana bahati kutokana na kuendelea kupanda kwa bei yake licha ya kupunguzwa kwa ushuru wa ziada (VAT) kwa asilimia nane mnamo Julai kwa kuwa kampuni za mafuta zimekataa kushusha bei.

Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu, ongezeko la bei ya gesi linalazimisha wengi kugeukia matumizi ya makaa na kuni, hali ambayo inachangia uchafuzi na uharibifu wa mazingira.

Huku haya yakiendelea, KRA tayari imetoa ilani ya kuongeza ushuru wa baadhi ya bidhaa kuanzia Oktoba 1, hivyo kuongeza mzigo wa gharama ya maisha kwa Mkenya.

Bidhaa ambazo zitaongezwa ushuru huo ni pamoja na pombe, maji ya chupa, sigara na vitafunwa kama vile biskuti na peremende.Mchanganuzi wa masuala ya uchumi, Ephraim Njega anaonya kuwa ukosefu wa mwongozo wa kiuchumi ndio kiini cha bei za juu na wanaoumia ni wananchi wa kawaida.“Kufanya maamuzi kiholela bila mwongozo ni hatari. Hii ndiyo ilikuwa desturi ya utawala ulioondoka na huu mpya unaonekana kufuata mkondo huo. Hali hii itafanya uchumi kuzorota zaidi na kuongeza mahangaiko kwa watu maskini. Hii inaweza kuchochea mgogoro wa kijamii, kisiasa na misukosuko,” asema Bw Njega.

    Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii