Waziri Mkuu wa Sweden wa chama cha Social Democratic Magdalena Andersson amewasilisha leo barua ya kujiuzulu. Hii ni baada ya muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia ambao unajumuisha chama cha siasa kali za kizalendo na kinachopinga uhamiaji kupata ushindi wa wingi mchache wa viti katika bunge la Sweden. Andersson alikutana na Andreas Norlen, spika wa Bunge la Sweden Riksdag lenye viti 349, ili kumfahamisha rasmi kuhusu kujiuzulu kwake.
Andersson ataendelea kuhudumu katika nafasi ya muda hadi serikali mpya itakapoundwa. Norlen anatarajiwa kumuomba kiongozi wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Moderate, Ulf Kristersson, kujaribu kuunda serikali ya mseto.
Kufuatia uchaguzi mkuu wa Jumapili, kundi la siasa za mrengo wa kulia lilipata viti 176 wakati kundi la siasa za wastani za mrengo wa kushoto na chama cha Social Democratic likiwa na viti 173.