Abiria afariki alipokuwa akipanda ndege ya KQ kuelekea Mombasa

Shirika la ndege la Kenya Airways limethibitisha kuwa abiria aliyepata matatizo ya kupumua alipokuwa akipanda moja ya ndege zake amefariki.

Katika taarifa Jumatano, KQ ilisema abiria huyo alitangazwa kuwa amefariki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) huku ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Mombasa ikiwa bado ardhini.

“Kenya Airways PLC inasikitika kutangaza kwamba abiria alipata matatizo ya kupumua jioni hii alipokuwa akipanda KQ612 ambayo iliratibiwa kuondoka hadi Mombasa saa 1900.

“Abiria huyo alitangazwa kuwa amefariki na wafanyikazi wa matibabu katika JKIA wakati ndege ilikuwa ingali chini,” KQ ilisema katika taarifa.

Hiki ni kisa cha tatu katika kipindi cha wiki nne zilizopita.

Shirika hilo mapema mwezi huu lilithibitisha kwamba abiria aliyekuwa kwenye mojawapo ya safari zake za ndege kuelekea New York kutoka Nairobi alikuwa ameaga dunia, ikiwa ni tukio la pili kama hilo kuripotiwa katika muda wa siku tisa.

Mwezi uliopita, iliripoti tukio lingine ambapo abiria alifariki kwenye mojawapo ya ndege zake kutoka New York kuelekea Nairobi.

Kulingana na shirika hilo la ndege, abiria huyo alipata matatizo ya kupumua saa saba baada ya ndege hiyo kupaa kutoka New York kabla ya kufariki. Msemaji wa familia alisema alikuwa na historia ya ugonjwa wa kisukari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii