Matumaini Ya Unga Wa Bei Nafuu Yafifia
Matumaini ya Wakenya kuwa gharama ya maisha ingeanza kushuka mara baada ya Rais William Ruto kuchukua madaraka yameanza kudidimia miongoni mwa Wakenya wengi.
Katika manifesto na kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 alioshinda, Rais Ruto aliahidi wapiga kura kwamba serikali yake itapunguza bei za bidhaa muhimu hasa unga wa mahindi na mafuta ndani ya siku 100 akiingia mamlakani.
Ahadi hizo ziliwapa Wakenya matumaini makubwa na alipoapishwa Jumanne wengi walitarajia angetangaza mikakati ya kuwaokoa kutokana na mfumko wa bei za bidhaa ambao unaendelea kuwalemea.
Katika hotuba yake ya kwanza, Rais Ruto hakutoa suluhu ya moja kwa moja kwa bei ya unga ambayo kwa wakati huu ni zaidi ya Sh200 kwa pakiti ya kilo mbili, badala yake akitangaza hatua alizosema ni za kuongeza mazao ya chakula ili kusaidia kupunguza bei.
Mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi na siasa, Ephraim Njega anasema Rais Ruto angetangaza ruzuku ya unga wa mahindi na ngano ili kushusha bei na kukinga wananchi wa tabaka la chini ambao wamelemewa na gharama ya juu ya maisha.
“Mataifa mengi yanatoa ruzuku ya bidhaa za kimsingi. Kilicho muhimu ni kuhakikisha inatekelezwa vizuri ili kuzuia ufisadi kuingizwa. Jukumu la kwanza la serikali ni kulisha raia wake,” akaandika Bw Njega kwenye Twitter.
“Changamoto za gharama ya maisha zinatokana na uzalishaji. Mikakati yetu wa kupunguza gharama ya maisha ni kwa kuwezesha wakulima kuzalisha chakula zaidi. Ubashiri wa mavuno ya mahindi mwaka huu ni chini ya magunia 30 milioni dhidi ya uzalishaji wa kawaida wa magunia 40 milioni. Kupungua kwa uzalishaji kunatokana na gharama ya juu ya uzalishaji,” akasema Rais Ruto baada ya kuapishwa katika uwanja wa Kasarani, Nairobi.
Bw Njega anasema ni sawa kuchukua hatua za kuongeza uzalishaji wa chakula kama suluhisho la muda mrefu, lakini kwa sasa wananchi wanapasa kusaidiwa kumudu gharama ya chakula.
Mnamo Juni 30, Rais Ruto aliwapa Wakenya matumaini kwa kuahidi kupunguza gharama ya maisha akiwa rais na kupuuza mtangulizi wake Uhuru Kenyatta aliyehusisha hali hiyo na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na janga la corona.
Baada ya kuapishwa Jumanne, Rais Ruto alisema hatua yake ya kwanza ni kupunguza bei ya mbolea ili kuwezesha wakulima kuzalisha chakula zaidi.
Ili kutimiza hilo, alipunguza bei ya gunia la mbolea ya kilo 50 kutoka Sh6,500 hadi Sh3,500 kuanzia wiki ijayo.
Hata hivyo, wananchi walivunjika moyo wakisema walitarajia aweke mikakati ya kupunguza bei ya unga mara moja.
“Kupunguza bei ya mbolea ni sawa lakini kwa sasa hakuna mvua na tunalemewa na bei ya unga. Tulitarajia afueni ya haraka,” akasema Daniel Larpaso, mkazi wa Nairobi.
“Tutaendelea kuumia kwa sababu afueni ya mbolea haiwezi kutufaidi sasa, pengine mwaka ujao iwapo mvua itanyesha,” akasema Brenda Kamau, mfanyabiashara wa nafaka Nairobi.
Kilichofifisha matumaini ya Wakenya kuhusu afueni ya gharama ya maisha, ni hatua ya Rais Ruto kutangaza kuwa ataondoa ruzuku ambayo serikali imekuwa ikitoa kudumisha bei za mafuta.
“Kuhusu ruzuku ya mafuta, walipa ushuru wametumia jumla ya Sh144 bilioni. Iwapo ruzuku hii itaendelea hadi mwisho wa mwaka wa kifedha, itagharimu mlipa ushuru Sh280 bilioni, sawa na bajeti yote ya maendeleo ya serikali,” alisema rais.
Alisema kwamba ruzuku hiyo ni ghali mno na inatumiwa vibaya. Kuondoa ruzuku hiyo kunamaanisha kuwa bei ya mafuta itaongezeka kwa zaidi ya Sh40 na kusababisha bei za bidhaa na huduma kupanda.
Kwa wakati huu bei ya petroli ni Sh159.12, dizeli ni Sh140.00 na mafuta taa ni Sh127.94 jijini Nairobi.
Mwezi Agosti, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA), ilisema ruzuku ilizuia bei ya petroli kupanda hadi Sh214.04 kwa lita, diseli Sh206.17 na mafuta taa Sh202.11 jijini Nairobi.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii