Kulikua na hali ya utulivu mkubwa katika sehemu mbalimbali nchini wakati wa kuapishwa kwa Rais William Ruto katika uwanja wa Kasarani.
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti katika kaunti ya Uasin Gishu mamia ya wakazi walijitokeza kushuhudia uapisho wa Dkt William Ruto kama rais wa tano, katika hafla ya kufana iliyohudhuriwa na zaidi ya marais 20 wa mataifa mbalimbali.
Kwa mapenzi yao kwa rais mpya, wengi wao hawakutishwa na kijibaridi na walikuwa katika mikahawa mbalimbali katika mji wa Eldoret kufuatilia uapisho wa rais huyo, ambao ulikuwa ukipeperushwa moja kwa moja kwenye runinga.
Wakazi hao walipiga kambi kando ya barabara kuu ya kuelekea Uganda, kufuatilia shughuli hiyo kwenye runinga kubwa iliyowekwa katikati ya mji wa Eldoret.
Waliojitokeza walitaka kuwa sehemu ya sherehe iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani, ambako rais anayeondoka Uhuru Kenyatta alimkabidhi mamlaka Dkt Ruto.
Eldoret ni mji wa nyumbani wa rais huyo mpya wa Kenya, ambaye anatoka eneo la Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu.
Aidha, wananchi kadhaa walikuwa wamevalia mmea wa Sinendet, ambao huvaliwa shingoni wakati wa sherehe na jamii ya Wakalenjin.
“Nimefurahi sana kushuhudia hafla hii ya kihistoria baada ya kusubiri kwa muda mrefu. Ni matumaini yangu kuwa, utawala huu utamjali mwananchi wa kawaida,” alieleza mkazi wa Chepkanga, Bw Kipkorir Koech.
Kwingineko, katika kaunti ya Mombasa ambayo ni ngome ya kinara wa ODM Bw Raila Odinga hali ilikuwa shwari na tulivu.
Licha ya biashara kadhaa kufungwa, shughuli ziliendelea kama kawaida, huku wengi wakionekana kulenga kujitafutia riziki.
Magari kadhaa yaliyokuwa yakiwasafirisha wafuasi sugu wa Dkt Ruto kutoka jiji la Mombasa, yaliondoka usiku wa kuamkia Jumanne.
Wakazi wa Mombasa walitulia makwao na kufuatilia hafla hiyo katika runinga zao. Wachache waliokuwa wakiuza walikuwa na runinga katika majengo ya biashara zao, walikuwa wakifuatilia hafla hiyo.