Madereva Bodaboda na Bajaji jijini Dar es Salaam, wametakiwa kujiamini na kutambua kuwa wana haki ya kujitafutia riziki kwa njia halali kwa kuzingatia Sheria za usalama Barabarani.
Hayo yamesemwa leo Desemba 20, 2021 na Kamanda wa Usalama Barabarani Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Abdi Issango wakati anazindua reflecta na vitambulisho vyenye namba ya siri kwa waendesha bodaboda na Bajaji wa Ukonga na vinginguti.
Amewaonya madereva hao kutojihusisha na matukio ya kihalifu na kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kuwa na leseni ya udereva, kupata mafunzo kwenye vyuo cha udereva na kuhakikisha vyombo vyao vimekamilika.
"Niwatake wote mnafanya kazi hii mjitambue kama Watanzania halali na mnayo haki ya kuishi na kujitafutia riziki kwa njia halali lakini mzingatia Sheria za usalama barabarani ili lengo la kupata kipato liweze kutimia, kwa njia halali," amesema Kamanda Issango.
Amebainisha kuwepo kwa baadhi ya madereva wasiokuwa waaminifu ambao hutumia kivuli cha kazi hiyo kuendeleza uhalifu kwa kuwapora watu na kukosesha sifa biashara hiyo inavyotakiwa.
"Tunawaomba badilikeni na itendeeni haki shughuli hii kama ambayo serikali ilivyokusudia kusafirisha abiria na kuimarisha ulinzi shirikishi ili watu wabaki salama na mali zao," amesema.
Naye Daniel Malagashimba Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwamkolemba Kata ya Kipungini jijini hapa, amewaomba kuzingatia ushauri waliyopewa ikiwemo kuvaa kofia ngumu wakati wote.
"Kuheshimu vivuko vya barabarani, Bodaboda wengi wanaendesha kama wamekata tamaa matokeo yake mnapata ajali tambueni afya ni bora kuliko fedha mnazokimbilia," amesema Malagashimba