Kiongozi mpya wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore amesema uchaguzi wa nchi hiyo unatarajiwa kufanyika mwaka 2024 au mapema zaidi ya hapo.
Akizungumza jana na Shirika la Utangazaji la Ufaransa (RFI), Traore amesema lengo la kufanya uchaguzi mwaka 2024 bado linawezekana. Amesema wana matumaini kwamba watarejesha utaratibu wa kawaida wa kikatiba hata kabla ya muda huo, iwapo hali itaruhusu. Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ilifikia makubaliano na kiongozi aliyepinduliwa, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba wa kuandaa uchaguzi ifikapo mwezi Julai mwaka 2024.
Damiba ambaye pia alichukua madaraka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Januari, alikubali kujiuzulu siku ya Jumapili na kwenda nchi jirani ya Togo. Aidha, vyombo vya habari vimeripoti kuwa ziara iliyokuwa ifanywe jana na ujumbe wa ECOWAS mjini Ouagadougou, imeahirishwa hadi leo.