Somaliland wakataa kuongeza muda wa rais

Viongozi wa upinzani wa jimbo la Somaliland ambalo lilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia wamekataa uamuzi usio halali wa kuongezwa muda wa rais kwa miaka miwili zaidi kabla ya kumalizika mwezi ujao.

Baraza lenye nguvu la wazee siku ya Jumamosi lilipiga kura kuongeza muda wa Rais Muse Bihi Abdi madarakani hadi 2024, likisema hatua hiyo itaumaliza mzozo wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu.

Akizungumza jana na waandishi habari mjini Hargeisa, kiongozi wa chama cha Wadani, Abdirahman Mohamed Abdullahi amesema hatua hiyo ni kinyume cha sheria na kwamba hapakuwa na mashauriano kabla ya tangazo hilo.

Uchaguzi wa urais ulipangwa kufanyika Novemba 13, mwezi mmoja kabla muda wa awali wa Rais Abdi haujamalizika. Kiongozi mwingine wa chama cha upinzani cha Haki na Ustawi, UCID Feysal Ali Warabe, amesema wataacha kutambua uhalali wa Rais Abdi kuanzia Novemba 13.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii