Rais William Ruto ametoa wito kwa bunge kubuni mikakati ya kuwahoji Mawaziri Bungeni, ili kufafanua sera za serikali na kujibu maswali kuhusu miradi yake.
Wakati wa hotuba yake alipofungua rasmi Bunge la 13 siku ya Alhamisi, Septemba 29, Rais Ruto alisema kuwa taratibu hizo zinanuia kuongeza uwajibikaji wa serikali, kwa raia wake.
"Natoa wito kwa bunge la kitaifa kuongeza hitaji la mawaziri kufika bungeni ili kufafanua ajenda za serikali, kuelezea sera na kujibu maswali ndani ya bunge katika kanuni zake,"Rais alisema.
Kwenye hotuba yake, Rais alisema utawala wake utakuwa na uwazi na pia kuipa fursa Bunge kutekeleza jukumu la uangalizi kwa nia ya kuhakikisha mali ya serikali inatumika vyema.
"Kupitia hatua hiyo, serikali yangu imejitolea kuipa Bunge mamlaka kwa kuheshimu jukumu lake la kuipiga msasa serikali. Ninaahidi kuongoza utawala ambao umejitolea kutekeleza usawa na haki kwa wakenya wote. Naahidi kuwa mtiifu na mwenye bidii, aliyejitolea kwa kila mkenya,” Rais Ruto alisema.