Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, John Mikel Obi, ameangika daluga zake kwenye ulingo wa soka akiwa na umri wa miaka 35.
Akitangaza maamuzi hayo, Mikel alisema “anaridhika na yote ambayo nimejivunia katika kipindi cha miaka 18 cha kusakata kabumbu.”
Nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia Chelsea taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012. Alichezea Nigeria mara 89 na akasaidia miamba hao kutwaa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2013. Alistaafu soka ya kimataifa mnamo 2019.
Umaarufu katika ulingo wa soka ulianza kumwandama Mikel kwa kipindi cha miaka 11 ambapo aliwajibikia Chelsea japo alihitaji jumla ya michuano 185 kabla ya kufungia kikosi hicho bao la kwanza.
Alichezea Chelsea mechi 249 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuongoza kikosi hicho kujizolea taji la Europa League, mataji mawili ya EPL, manne ya Kombe la FA na mawili ya Carabao Cup.
Kikosi chake cha mwisho kuchezea ni Kuwait SC kilichoagana naye mnamo Novemba 2021 baada ya miezi mitano pekee.
Jina la Mikel lilianza kutambulika katika ulingo wa kandanda mnamo 2005 huduma zake zilipoanza kung’ang’aniwa na Manchester United pamoja na Chelsea kutoka kambini mwa Lyn Oslo jijini Norway.
Alibatilisha maamuzi ya kutua ugani Old Trafford mnamo 2005 na kuingia katika sajili rasmi ya Chelsea mnamo 2006. Aliondoka uwanjani Stamford Bridge mnamo 2017 na kuyoyomea China kuvalia jezi za Tianjin Teda. Amewahi pia kuchezea Trabzonspor ya Uturuki na vikosi viwili vya ligi ndogo nchini Uingereza – Middlesbrough na Stoke City.