Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amefungua rasmi dirisha la ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (Samia Scholarship) ambapo wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita, wataanza kuomba kesho.
Ufadhili huo utahusisha ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, posho ya vitabu na viandika, mahitaji maalum ya vitivo, vifaa saidizi kwa wenye mahitaji maalum na bima ya afya.
Profesa Mkenda ametangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo leo Jumanne Septemba 27, 2022 katika mkutano wa wadau wa elimu wa kujadili rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu.
Amesema majina ya wanafunzi waliopata ufaulu wa juu yatatangazwa leo katika tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).