Muungano wa vyama vinavyoegemea mrengo wa kulia unaoongozwa na chama cha Giorgia Meloni cha Brothers of Italy nchini Italia, unatarajiwa kushinda katika uchaguzi wa serikali mpya nchini humo.
Kura za maoni zilionyesha kuwa muungano huo ulionekana kushinda na takribani 45% ya kura. Kura hizo zitatosha kuuwezesha muungano huo kuwa na wingi wa viti bungeni. Matokeo yanayotarajiwa yanaashiria kupanda kwa kasi kwa chama cha mrengo wa kulia cha Meloni, ambacho kilipata asilimia 4 pekee ya kura katika uchaguzi uliopita.
Chama cha Brothers of Italy sasa kinatarajiwa kushinda 22.5-26.5% ya kura. Meloni anaweza kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Italia. Idadi ya wapiga kura ilikuwa inaelekea kuwa ya chini kabisa huku zaidi tu ya nusu ya wapiga kura wakipiga kura hadi masaa manne kabla ya zoezi hilo kufungwa. Uchaguzi huo mkuu wa ghafla ulichochewa na kujiuzulu mwezi Julai kwa waziri mkuu anayemaliza muda wake Mario Draghi.