Ruto Aita Wahubiri Ikulu Kwa Maombi
RAIS William Ruto jana Jumapili aliruhusu viongozi wa makanisa kufanya maombi spesheli ya kutakasa ikulu ya Nairobi huku akijiandaa kuanza kutumia makao hayo ramsi ya kiongozi wa nchi.
Rais Ruto alisema utakaso huo ulihitajika kwa kuwa utawala wake utakuwa ukitegemea nguvu za maombi.
Akizungumza baada ya ibada iliyohudhuriwa na viongozi wa makanisa na wa muungano wa Kenya Kwanza katika ikulu, Rais Ruto aliwaomba wahubiri hao kutakasa jengo na uwanja wa makao hayo ya rais.
“Baada ya ibada hii, kutakuwa na sehemu ya pili ambayo haitakuwa na utaratibu kama ya sehemu ya kwanza. Tutauliza mapasta 30 au 40 wale wakuu kuombea jengo hili na makazi, na ofisi ili Mungu aweze kutupatia suluhu ya nchi hii,” Rais alisema.
“Msiondoke kwa haraka. Ombeeni baraka uwanja huu na mzunguke kote hapa mkitakasa, hata katika shamba, kila mahali. Wale wanaozungumza kwa ndimi, tafadhali fanyeni hivyo, ili ijulikane kwamba wapangaji wapya wamefika,” alisema Rais Ruto.
Alisema alikuwa ameagiza wakuu wa usalama na wafanyakazi wa ikulu kuwaruhusu viongozi hao kuzunguka kila kona kufanya maombi.
Rais Ruto aliwataka viongozi hao waendelee kuombea serikali ili ifaulu katika mipango yake.
“Ninataka muombee mpango wetu ili wale walio na njaa tuweze kuwapatia chakula, wale wasio na makao tuweze kuwajengea nyumba, na wale walio wagonjwa tuweze kuwa ya mpango wa afya kwa wote,” akasihi kiongozi wa nchi.
Rais Ruto aliwahimiza Wakenya kuendelea kudumisha amani ambayo alisema imefanya nchi kuheshimiwa kote ulimwenguni.
“Kenya imesifiwa kote ulimwenguni kwa kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Huu ulikuwa ushindi kwa nchi nzima,” akasema.
“Uchaguzi ulikuwa ushindi wa Kenya. Tumepongezwa kote ulimwenguni kwa sababu ya uchaguzi wa amani.”
Kiongozi wa nchi alisema kwamba kuna watu wengi ambao waliombea amani Kenya na hali hiyo inafaa kudumishwa.
“Huu ni ushindi wa Kenya, kwa uchaguzi wa amani na uwazi,” akaongeza Rais Ruto.
Kuhusu tatizo la ukame, Rais alisema serikali inashirikiana na magavana kuweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
Rais Ruto alisema kwamba serikali itakabiliana vikali na visa vya ukosefu wa usalama katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa na ujangili ambao umefanya maafisa wa usalama na raia kupoteza maisha.
“Serikali itafanya kila iwezalo kuleta amani ya kudumu katika Kaunti ya Turkana kwa kuangamiza ujangili katika eneo hilo na maeneo mengine yanayokumbwa tatizo la wizi wa mifugo,” akasema Rais.
Mnamo Jumamosi, watu 11 wakiwemo maafisa 8 wa polisi waliuawa na wezi wa mifugo Turkana.
Maafisa hao walikuwa wakisaka majangili waliokuwawameiba ng’ombe. katika kijiji kimoja Turkana Mashariki.
“Tunawahimiza muombee vikosi vyetu vya usalama ili viweze kutekeleza majukumu yao ya kudumisha usalama wa kila Mkenya. Wiki jana niliagiza wapewe uhuru wa kusimamia pesa ili wasiwe na sababu ya kutotekeleza majukumu yao,” alisema.
Alisema Naibu Rais Rigathi Gachagua atakutana na magavana na wakuu wa idara tofauti kujadili mbinu za kukabilia na ukame ambao unaathiri zaidi ya watu 3.1 milioni katika kaunti za Kaskazini na Kaskazini Mashariki ya Kenya.
Dkt Ruto alisema katika wiki chache zijazo, atataja serikali ambayo itatekeleza ajenda za maendeleo katika sekta tofauti.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii