Waziri mkuu wa mpito nchini Mali kanali Abdoulaye Maiga, ameishtumu Ufaransa kwa kulitelekeza taifa hilo. Wakati wa hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maiga amesema kuwa Mali imesalitiwa baada ya jeshi la Ufaransa kujiondoa nchini humo mapema mwaka huu. Ufaransa imekuwepo nchini Mali tangu 2013 kusaidia taifa hilo katika mapambano yake dhidi ya waasi wa itikadi kali.
Vikosi vya Ufaransa vilikaribishwa kwa furaha vilipowasili Mali miaka tisa iliyopita, lakini uhusiano huo sasa umedorora. Mnamo mwezi Aprili, rais Emmanuel Macron alitangaza kuwa vikosi vya Ufaransa vitajiondoa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Maiga ameilaani Ufaransa kwa kile alichokiita uamuzi wa upande mmoja wa kuvihamishia vikosi vilivyosalia hadi nchi jirani ya Niger, akisema Ufaransa inajihusisha na ukoloni mamboleo na udhalilishaji.