Wamatangi Azuru Afisi Mbalimbali Za Kaunti Akiahidi Kuimarisha Kiambu

Gavana  mpya wa Kaunti ya Kiambu, Kimani Wamatangi, alizuru afisi za kaunti ndogo ya Thika mnamo Jumanne ili kupata picha halisi ya hali ya kazi.

Gavana  huyo aliyeandamana na maafisa wakuu wa kaunti alifika mjini Thika, majira ya saa mbili za asubuhi huku akitembelea karibu kila afisi mchana kutwa ili kuelewa jinsi wafanyakazi wanavyoendesha shughuli zao.

Baadhi ya afisi alizozuru ni ile ya fedha, ya maji, mazingira, na hata uchukuzi.

Mchana kutwa gavana huyo alichukua muda wake wote akitaka kufahamu mengi jinsi kaunti ya Kiambu ilivyokuwa ikiendeshwa na mtangulizi wake Dkt James Nyoro.

Mnamo Jumatatu, gavana huyo alichukua muda wake akizuru kila eneo katika afisi zote za makao makuu ya Kiambu.

Wafanyakazi wengi walibaki kutazama tu na macho kujionea jinsi maafisa wakuu walivyozunguka kila afisi ili kumdokezea yaliyokuwa yakiendelea hapo awali.

Bw Wamatangi aliwahakikishia wafanyakazi wote waendelee kutekeleza wajibu wao bila uwoga wowote kwani azma yake kuu ni kuboresha huduma zinazotolewa na serikali ya kaunti kwa manufaa ya wananchi.

Mnamo Alhamisi iliyopita ya Agosti 25, 2022, wakati wa kula kiapo cha kuingia afisini alitoa ahadi chungu mzima kwa kusema atatekeleza wajibu wake bila mapendeleo.

Alidai kuwa utendaji kazi utamhusisha kila mkazi bila kubagua yeyote.

“Lengo langu kuu ni kuboresha huduma Kiambu na kuimarisha maendeleo. Kwa hivyo kila mmoja atapata nafasi yake,” alifafanua wakati wa hotuba yake kwa wananchi katika uwanja wa Kirigiti.

Alitoa ahadi kwa wakulima kuwa watapokea pembejeo za kuboresha kilimo chao.

Aliwapa matumaini wawekezaji kwa kusema ya kwamba watapewa nafasi kuwekeza katika kaunti ya Kiambu.

Alisema ataboresha hali ya afya kwa kufanya juhudi kuona ya kwamba dawa zinapatikana katika hospitali zote katika kaunti.

Alidokeza pia kuhusu vijana kwa kusema watatafutiwa njia ya kwenda katika vyuo vya kiufundi kwa mafunzo ya kuboresha maisha yao kwa kufanya kozi tofauti kwenye vyuo hivyo.

    Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii