Mfalme Charles III Afanya Ziara kwa mara ya kwanza Ireland Kaskazini

Mfalme Charles III amefanya ziara yake ya kwanza Ireland ya Kaskazini tangu alipovikwa taji la ufalme. Mfalme Charles anazuru mataifa yote manne ya Ufalme wa Uingereza kabla ya mazishi ya kitaifa ya mama yake, Malkia Elizabeth II wiki ijayo.

 

Ndege iliyombeba Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 73 ilitua mjini Belfast, ikitokea Edinburgh, ambako jeneza la mwili wa malkia lilipelekwa baada ya kifo chake Alhamisi wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 96.

 

Jeneza hilo linasafirishwa jioni hii kuelekea London, ambako umati mkubwa watu unatarajiwa kutoa heshima zao kuanzia Jumatano jioni hadi siku ya mazishi yake Jumatatu asubuhi.

 

Wakati akiwa mrithi wa kiti cha Ufalme, Charles alifanya ziara 36 Ireland Kaskazini, ambayo historia yake ya karibuni imeharibiwa na machafuko ya kimadhehebu kuhusu utawala wa Uingereza na ambako makubaliano tete ya amani yamekuwa yakiheshimiwa tangu mwaka wa 1998.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii