Mchezaji wa Man City Benjamin Mendy Afutiwa Shtaka la Ubakaji

Mchezaji wa Manchester City, Benjamin Mendy hakupatikana na hatia katika kesi ya kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 19.

Uamuzi huo ulitolewa na jaji wa Mahakama ya Chester Crown nchini Uingereza mnamo Jumanne, Septemba 13, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutoa ushahidi wa kutosha dhidi ya nyota huyo.

Mshitakiwa mwenza wa Mendy, Louis Saha Matturie, pia alifutiwa mashtaka mawili ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono dhidi ya mwanamke huyo.

Jaji Stephen Everett alionya alionya baraza la maamuzi dhidi ya kueneza uvumi kuhusu upande wa mashtaka kuamua kutofuata maamuzi kuhusiana na kesi hiyo na badala yake kuwataka kwa uaminifu kuwahukumu washtakiwa kwa mashtaka mengine ambayo bado yanawakabili.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, anaripotiwa kutekeleza kitendo hicho nyumbani kwake katika eneo la Cheshire, Uingereza kati ya Oktoba 2020 na Agosti 2021.

Hata hivyo, bado beki huyo Mfaransa anakabiliwa na mashtaka mengine saba ikiwemo ya kujaribu kubaka na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake sita.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa Mendy ni "mwindaji" ambaye aligeuza harakati za kuwatafuta wanawake kufanya ngono kuwa mchezo.

Matturie, rafiki yake Mendy, naye anadaiwa kuwa ndiye alikuwa na kazi ya kutafuta wanawake wa kufanya mapenzi na Mendy.

Matturie alikanusha mashtaka sita dhidi yake ya ubakaji na matatu ya unyanyasaji wa kingono yanayohusiana na wasichana saba.

Wawili hao wanajitetea wakisema kuwa iwapo ngono yoyote ilifanyika na wanawake au wasichana, ilitokana na makubaliano.

Kufuatia kesi hiyo, Manchester City ilifuta bidhaa zote zenye jina la Benjamin Mendy kutoka kwa tuvuti yake rasmi na duka la mkononi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii