Wabunge Na Maseneta Kufanya Kikao Cha Kwanza Septemba 8.

Vikao vya kwanza vya Bunge la Kitaifa na Seneti vitafanyika mnamo Alhamisi,  Septemba 8, 2022 ambapo wajumbe katika mabunge hayo wataapishwa kisha wawachague maspika wao.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuchapisha ilani katika gazeti rasmi la serikali ya kuitisha vikao vya kwanza vya Bunge la 13 baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9.

Vikao hivyo, vitafanyika katika kumbi za mijadala za mabunge hayo zilizoko katika majengo ya bunge, Nairobi kuanzia saa tatu asubuhi (9.00 am).

“Kwa mujibu ya mamlaka yaliyoko katika kipengele cha 126 (2) cha Katiba ya Kenya, miye Uhuru Kenyatta, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, natangaza kuwa kikao cha kwanza cha Seneti na Bunge la Kitaifa kitafanyika katika majengo ya bunge mnamo Septemba 8, 2022 saa tatu asubuhi,” notisi hiyo.

Hatua hiyo sasa inaashiria kuanza kwa shuughuli katika mabunge hayo mawili kuelekea kuanza kwa kazi rasmi za bunge la 13.

Kwanza, makarani wa mabunge hayo mawili wataongoza shughuli ya kuapishwa kwa wabunge na maseneta wateule.

Baada ya muda, wabunge hao watapiga kura ya kuwachagua maspika wao kupitia kura ya siri.

Hata hivyo, kabla ya maseneta kuapishwa, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itahitaji kuchapisha majina ya maseneta wateule katika gazeti rasmi la serikali pamoja na wale maalum.

Vile vile, tume hii inatarajiwa kuchapisha majina ya wabunge na maseneta maalum katika gazeti rasmi la serikali, kabla ya wao kutambuliwa rasmi, kuapishwa na kushiriki katika uchaguzi wa maspika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii