Johnson" Nitamuunga mkono mrithi wangu Liz Truss"

Waziri Mkuu anaeondoka nchini Uingereza Boris Johnson ameapa kumuunga mkono mrithi wake Liz Truss katika kila hatua atakayoipiga kwenye kazi zake. Katika hotuba yake ya mwisho kama Waziri Mkuu aliyoitoa katika ofisi yake ya Mtaa wa Downing, Boris amesema muda umefika wa kila mtu kumuunga mkono kikamilifu Liz Truss. Kiongozi huyo wa Uingereza aliyetangaza nia yake ya kujiuzulu miezi miwili iliyopita, anatarajiwa kukutana na Malkia Elizabeth wa Uingereza ili kuanza mchakato wa kukabidhi madaraka kwa Truss. Johnson amewatolea mwito pia wanachama wa chama chake cha Conservative kuweka kando tofauti zao ili kukabiliana na mgogoro wa nishati ambao ni miongoni mwa changamoto atakazokutana nazo Truss katika majukumu yake. Truss aliyetangazwa kiongozi wa chama cha Conservative hapo jana anatarajiwa kuteuliwa kama Waziri Mkuu katika mkutano wake na Malkia hapo baadae.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii