Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MCSL), Erick Hamisi amesema ujenzi wa meli ya MV Mwanza umefika asilimia 71 na inatarajiwa kuanza huduma mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Amesema hayo akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo wakati wa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
Katika ziara hiyo, Kinana ametembelea eneo inapojengwa meli hiyo na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo.
Kwa Mujibu wa Hamisi, meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 23.